ADHIMISHO LA MISA TAKATIFU KWA DARAJA TAKATIFU LA USHEMASI JIMBO KUU KATOLIKI ARUSHA
Tarehe 9 Januari 2025, Parokia ya Tokeo la Bwana Burka, Jimbo Kuu Katoliki Arusha, yaadhimisha Daraja la Ushemasi kwa Mashemasi Saba. Parokia hiyo imekuwa mwenyeji wa Adhimisho la Misa Takatifu kwa ajili ya Daraja Takatifu la Ushemasi. Ibada hii Takatifu imeongozwa na Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Isaac Amani, na kuhudhuriwa na waumini wengi kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Katika adhimisho hili, Mashemasi saba walipokea Daraja Takatifu la Ushemasi. Mashemasi hao ni Shemasi Emiliano Silayo, Shemasi Evance Riziki, Shemasi Frank A. Monoruwa, Shemasi Gilbert Manase, Shemasi John Kilasa, Shemasi Joseph Mangi na Shemasi Thadei Kilasara. Kupokea daraja hili ni hatua muhimu kwa mashemasi hao kuelekea Upadrisho, hatua ya mwisho katika maisha ya wito wao wa kipadre.
MANENO YA BUSARA KUTOKA KWA MHASHAMU ASKOFU ISAACK AMANI
Katika mahubiri yake, Mhashamu Askofu Isaac Amani aliwahimiza mashemasi hao, pamoja na waumini wote, kuishi kwa uaminifu na kutambua uzito wa wito wao. Alisisitiza kwamba kila mwenye wito mtakatifu ana jukumu la kuishi kwa kujitoa, kwa uaminifu na kwa huduma ya Mungu na wanadamu.
“Nawasihi wote wenye Miito mitakatifu tuishi kwa Neno la Mungu na kulitumikia kwa bidii. Tukumbuke kuwa Neno la Mungu ni taa inayotuongoza kuelekea Ufalme wa Mbinguni,” alisema.
Aidha, aliwataka waumini kuacha tabia ya ubinafsi, iwe katika familia, makanisa, maofisini au jamii kwa ujumla. Alisema kwamba ubinafsi huzuia upendo wa kujitoa kwa ajili ya wengine, kinyume na mfano wa Yesu Kristo aliyetoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wa wanadamu.
MAMBO MATATU MUHIMU KWA MASHEMASI
Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani aliwakumbusha mashemasi hao kuzingatia mambo makuu matatu katika maisha yao ya wito:
1. Kumtii Kristo pasipo masharti.
2. Kuwajibika katika utume waliokabidhiwa na Mungu Baba.
3. Kuishi kwa nidhamu na uaminifu wakimfuata Yesu Kristo.
Aliwataka kuyatimiza yote waliyoyaahidi kwa moyo wa dhati na kujitambua kuwa wamechaguliwa kutangaza Injili kwa hiari yao wenyewe.
“Tuishi kwa heshima, nidhamu na kujitenga na maovu. Tukumbuke kuwa tumekubali kwa hiari kuitangaza Injili ya Kristo kwa njia ya miito mitakatifu iwe ni katika ndoa au utume wa kipadre,” alisisitiza.
Adhimisho hili la Daraja Takatifu la Ushemasi limeacha alama ya kiroho kwa mashemasi hao na waumini walioshuhudia. Hii ni ishara ya ukuaji wa kiimani na huduma endelevu katika Jimbo Kuu Katoliki Arusha.