JAMBO LA MSINGI

Jambo la msingi hapa ni udumifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wakristo Wakatoliki wanapofunga ndoa, wanapeana ahadi ya kupendana na kuheshimiana katika maisha yao yote! Wanapeana ahadi ya kuwapokea kwa mapendo watoto watakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake. Wanandoa wanapeana ahadi ya kuwa waaminifu katika taabu na raha, katika magonjwa na afya, kwa kupendana na kuheshimiana siku zote za maisha yao! Ndoa halisi ni pale, wanandoa wanapoadhimisha Jubilei ya Miaka 25, Miaka 50, Miaka 75 ya udumifu wao katika maisha ya ndoa na familial Huu ni wakati muafaka wa kushikana mikono kwa furaha na moyo wa shukrani, kwa kusindikizwa na neema na baraka za Mungu katika maisha yao hadi kufikia wakati huo. Hata hivyo yataka moyo! Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iwe ni dira na mwongozo wa familia za Kikristo.

Sisi Waamini tunatakiwa tujichotee nguvu, neema, baraka na utakatifu wa maisha, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu adili na matakatifu. Sisi Waamini tulioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, tuendeleze mema na mazuri tuliyofundishwa wakati wote wa katekesi na maandalizi ya kupokea Sakramenti ya Kipaimara na wala huo usiwe mwisho wa kuhudhuria Kanisani.

UJUMBE WA PENTEKOSTE KWA MWAKA 2019.

Sherehe ya Pentekoste, (siku hamsini baada ya Pasaka) ni adhimisho la kuzaliwa Kanisa. Yesu Mfufuka na utabiri wa nabii Yoeli vilitimia.

Kabla ya kupaa mbinguni Yesu aliwaagiza mitume wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba ya kubatizwa katika Roho Mtakatifu Mndo. 1:4-5.

Kwa nguvu za Roho Mtakatifu wanafunzi wanakuwa mashuhuda na waenezi wa Injili mpaka miisho ya dunia. Nabii Yoeli alishatabiri Siku ya Mwenyezi Mungu ambapo maajabu matatu yangetokea:

Mosi, Kumiminwa kwa Roho Mtakatifu,

Pili, Kutokea ishara na miujiza na

Tatu ni Wokovu kwa wote wenye kutubu na kuliitia jina la Bwana. Yoeli 2:28-32. Tuombee Familia na jumuiya zetu zijazwe mapaji 7 ya Roho Mtakatifu.

Siku ya Pentekoste, ndipo Mwenyezi Mungu aiipotimiza ahadi ya kumimina Roho Mtakatifu kwa waliomwamini Yesu na ndtvyo Kanisa lilivyozaliwa \”Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka\” Kwa mara ya kwanza tangu mafarakano ya Babeli binadamu waliunganishwa kwa lugha iliyoleta Umoja; watu wa lugha na mataifa mbalimbali wakaelewa kwa kuwa hawakuhitaji mkalimani bali kila mmoja aliwasikia mitume kwa lugha yake mwenyewe Mndo 2:6. Mtume Petro alikuwa na kazi kubwa ya kueleza sababu ya mabadiliko hayo makubwa yaliyotokea ghafla. Alinukuu maneno ya Nabii Yoeli akieleza ahadi ya Mungu iliyotimizwa: \”Nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto\” Kwa maneno mengi Petro alishuhudia jinsi Yesu wa Nazareti alivyodhihirishwa na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara kati ya watu na jinsi alivyosulibishwa kwa mikono ya watu wabaya na kuuawa.

Yesu huyo Mungu alimfufua na mitume ndio mashahidi wake. \”Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ite ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia \”Mndo 2:32-33. Watu walichomwa mioyo wakataka kujua wafanye nini. Petro aliwaambia: \”Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie \”Mndo. 2:38-39). Kwa mujibu wa ubatizo wetu, leo twaadhimisha kuzaliwa kwetu katika Kanisa na kupewa ahadi ya kurithi baraka na ahadi za milele tukiwa taifa la Agano Jipya lenye kuunganishwa na Roho Mtakatifu. \”Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inayoviungamanisha viumbe vyote hujua maana ya kila sauti\” Hek.l :7.

Mwenyezi Mungu ametimiza ahadi ya kutupelekea Mwanaye ili atukomboe.

Amempeleka Roho Mtakatifu ili atutakase, atuunganishe na kutujuza maana ya kila sauti. Yesu alisema Roho Mtakatifu \”Atawafundisha yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia\” Yoh.14:26. Roho Mtakatifu hutuwezesha kutimiza ahadi zetu.

Tuyafuate maongozi yake daima kwani yeye ndiye Msaidizi wetu mkuu. Je! Sisi waamini tumekuwa waaminifu kwa ahadi zetu kwa Mungu? Tunayo ahadi ya Ubatizo.

Mtume Petro anaeleza Ubatizo kuwa si \”shauri la kuondoa uchafu mwiiini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi\” 1Pet. 3:21-22. Kwa ubatizo twawekwa wakfu kwa Mungu.

Tunayo ahadi ya wazazi wenye kuombea watoto ubatizo: \”Je! Mnapomwombea mtoto wenu ubatizo, mwafahamu wajibu mnaopokea, yaani kumfundisha imani apate kushika amri za Mungu na kumpenda jirani kama Kristo alivyotufundisha?\” Hujibu: Twafahamu. Idadi kubwa ya watoto hawajui sala wala misingi ya imani. Tunayo ahadi ya msimamizi wa ubatizo: \”Je ? Uko tayari kuwasaidia wazazi wa mtoto huyu katika wajibu wao?\” Hujibu: \”Niko tayari\”. Wangapi hufuatilia malezi ya watoto waliowasimamia? Baadhi ya wasimamizi ni wa kupiga Picha na sherehe. Wazazi na wasimamizi huhimizwa kumsaidia mtoto atembee daima kama mtoto wa nuru, adumu katika imani. Watoto wengine hupelekwa kwenye mahubiri ya kuvuruga imani! Wajibu wa kuwafundisha watoto sala za asubuhi na za jioni, maadili ya kikristo na mfano mwema wa kuishi maisha ya sakramenti ndiyo malezi na majukumu ya wazazi na wasimamizi wa ubatizo.

Kila Jumuiya Ndogo Ndogo ya Kikristo iwe na utaratibu wa kuwafundisha watoto sala na maadili ya Kikristo kupitia Shirika la Utoto Mtakatifu. Kwa hiyo mtoto asali nyumbani na katika Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Watakaoandikishwa kwa mafundisho ya Komunyo ya kwanza wawe wanafahamu sala za asubuhi na jioni. Tunayo ahadi ya wanaofunga ndoa: \”Je! Mko tayari kuwapokea kwa mapendo watoto mtakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa lake?\” Hujibu \”Tuko tayari\” Ahadi hiyo ni deni kwa Mungu, kwa Kanisa na kwa mtoto. Baadhi ya wazazi hupinga taratibu za kumlea mtoto katika imani kwa wakati wake. Mfano kutomfundisha mtoto sala, kumkataza kuingia shirika na kumwaminisha kwamba \”tuition\” ina maana zaidi kuliko mafundisho ya dini. Kwa kuchelewesha watoto mafundisho ya Komunyo na Kipaimara ieo hii tunao vijana Sekondari na Vyuo vikuu ambao hawajapata Komunyo ya kwanza na Kipaimara!

Zipo ahadi za miito: Maagano ya Ndoa Takatifu na Maisha ya Nadhiri. Binadamu huweka ahadi rasmi kwa Mungu kujitoa nafsi kwa mwenzi wa maisha au kwa Mungu mwenyewe kufuata taratibu za wito mtakatifu. Hizo ni ahadi kwa Mungu na ahadi ni deni. Tunaposherehekea Pentekoste tuombe miminiko la Roho Mtakatifu kwa waamini wote.

Tutambue kwamba \”Katika ubatizo mmoja Sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja\” 1Kor.12:13. Kila mmoja amejaliwa karama na vipaji tofauti kwa ajili ya huduma kwa wote.

Tukisukumwa na upendo na ukarimu wa kimungu, kila mmoja wetu huleta talanta zake katika jumuiya na hivyo kujenga umoja. Sio mashindano na utengano. Uwepo wa ufalme wa Mungu katika familia au jumuiya hudhihirika kwa matunda ya Roho Mtakatifu: \”Upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi\” Gal.5:22-23. Pamoja na matunda hayo ya Roho Mtakatifu twapaswa kubadilika kifikra na kitabia ili tutengeneze mazingira ya kuzaa matunda hayo. \”Ni lazima tuisulibishe miili na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho\” Gal.5:25. Mti hujulikana kwa matunda yake.

Tumepewa Roho Mtakatifu ili atutakase na kutupa amani ya kweli tuweze kuwa vyombo vya kueneza umoja aliotuombea Yesu. Ishara na miujiza ionekane kwa waamini kuelewa kwamba \”watao-okolewa kwa kuondolewa dhambi zao\” Lk. 1:.77. Turejee ahadi zetu, tubadilike na kuishi tunu za Injili ili tuwe Wakristo Wakatoliki kweli. Turejee maisha ya Sakramenti ili tuwe Wakatoliki hai wenye kujitambua kuwajibika na kushirikiana katika Kristo kwa matendo, kama wakristo wa kwanza walivyofanya. Wao wakiongozwa na Roho Mtakatifu walikuwa na mtindo wa maisha uliowatofautisha na watu wengine: \”Walishirikishana mali zao wakijali mahitaji ya kila mmoja wao. Walikutana Hekaluni iii wapate mafundisho ya mitume, walimega mkate katika nyumba zao na wakakishiriki chakula (Ekaristi) kwa furaha na moyo mkunjufu. Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa \”Mndo.2:45-47. Hayo ndiyo matendo makuu yaliyoimarisha waamini wakawa na nguvu ya kushuhudia imani na kueneza Injili katika changamoto za kijamii kama siasa na uchumi. Sisi Wana-arusha tunajiandaa  kuadhimisha miaka 60 ya imani ifikapo 2023. Tumeandaa Mpango Mkakati utakaotuwezesha kusafiri pamoja kijimbo.

Dira ya mpango huo ni: Familia ya Mungu inayoishi kadiri ya Injili ya Kristo\”

Utume wake: \”Kujenga Familia ya Mungu yenye upendo, moyo wa utambuzi, uwajibikaji na ushirikiano wa matendo kwa kutangaza Injili na kutoa huduma za kiroho na kimwili kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki\”. Tunu msingi: Upendo, Umoja, Haki na amani, Kuheshimu na kulinda uhai na hadhi yake, Uwazi na uwajibikaji, Maisha ya Sala na Ubunifu.

Aidha tumeweka Malengo Mkakati saba (7):

 i) Kuimarisha Imani Katoliki, 

ii).  Kuimarisha Maadili ya Kikristo 

iii).  Uelewa wa Sheria,

iv)  Kuboresha Uchumi, Elimu na Afya  v).  Ujenzi wa Kanisa Kuu  vi).  Kuwezesha Jimbo kutoa huduma na 

vii).  Gharama za kutekeleza Mpango Mkakati 2019-2023.

Ni matumaini yetu kwamba Mpango Mkakati huo utatusaidia kuimarisha imani na maendeleo yetu. Kwa bahati tunajiandaa kwa uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri Walei (2019). Mipango mizuri bila viongozi wenye sifa na ari ya maendeleo ni ndoto tu. Kutakuwepo na Semina za kujiandaa kwa uchaguzi wa viongozi wenye sifa za kikanisa watakaosimamia Mpango Mkakati katika roho ya kuwajibika na kushirikiana katika Kristo. Watakaochaguliwa watapewa semina ya kuwaandaa kabla ya kusimikwa. Uongozi ni utumishi. Tuendelee na sala ya kuombea uchaguzi wa viongozi walei ngazi zote ili tuyafikie malengo ya Mpango Mkakati.

Nawatakieni baraka na wingi wa Roho Mtakatifu katika sherehe hii ya kuzaliwa Kanisa na pia kuzaliwa kwetu katika Ubatizo. Tumewekwa wakfu, tuishi kitakatifu na tutakatifuze malimwengu kwa kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu nyumbani na katika huduma zetu zote. Roho Mtakatifu awaongoze watoto wetu watabiri wakiangaziwa na malezi mazuri, wazee waote ndoto za kudhihirisha ukomavu wa imani na vijana wawe na maono yenye kumtanguliza Mungu na wokovu wanapopangilia maisha. \”Waipeleka Roho yako, ee Bwana; Nawe waufanya upya uso wa nchi\” Zab.104:30 Katika roho ya Mwondoko: Kujitambua, Kuwajibika na Kushirikiana katika Kristo kwa Matendo.

 Askofu Mkuu Isaac Amani Massawe.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha.