Maelezo Mafupi ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha

Jimbo Kuu Katoliki Arusha lilianzishwa tarehe 1 Machi 1963 baada ya Jimbo Katoliki  Moshi kugawanywa. Lilisajiliwa rasmi kuwa Bodi ya Wadhamini ya Jimbo Katoliki  Arusha tarehe 17 Juni 1965. Mnamo tarehe 16 Machi 1999 Jimbo lilipandishwa hadhi kuwa jimbo kuu na hapo ndipo likawa Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Lilisajiliwa rasmi kuwa Bodi ya Wadhamini ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha mnamo terehe 22 Julai 2002 na vile vile kusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani kama Chama (Mkusanyiko wa Waumini) kwa namba SO No. 8848. Makao makuu ya Jimbo Kuu yapo kwenye eneo la Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu.

Jimbo Kuu Katoliki Arusha limeenea eneo lote la Mkoa wa Arusha na sehemu ya Mkoa wa Manyara, kaskazini – mashariki mwa Tanzania. Lilipewa jina kutokana na jiji la Arusha ambalo liko chini ya Mlima Meru ambao ni mlima wa pili kwa urefu hapa Tanzania baada ya Mlima Kilimanjaro.

Jimbo Kuu Katoliki Arusha ni kubwa kuliko Jimbo lo lote hapa Tanzania likiwa na eneo la kilomita za mraba zipatazo 67,340. Linanyooka kuelekea kusini kupitia Nyika za Wamaasai  (Maasai Steppes) hadi Kiteto, likipakana na Jimbo Katoliki Morogoro na JImbo Katoliki Kondoa na upande wa magharibi kupitia Monduli  kuelekea Bonde la Ngorongoro kupitia Olduvai Gorge, kuvuka nyika za Serengeti na kupakana na Jimbo Katoliki Musoma na Jimbo Katoliki Shinyanga. Linanyooka kaskazini – magharibi hadi Loliondo mpakani na Jimbo Katoliki Ngong nchini Kenya na kusini-mashariki likipakana na majimbo Katoliki  Moshi, Same na Tanga.

Makabila

Kuna makundi ya makabila kadhaa kwenye Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Makabila makuu ni: Wamasai, Waarusha, Wameru, Wapare, Wachaga, Wasonjo na Wairaqw.  Kutokana na kushamiri biashara ya utalii, machimbo na biashara zingine zinazofanana na hizo na vile vile kuwa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna makabila mengine kutoka sehemu mbali mbali za nchi na hata nje ya nchi. Lugha ya mawasiliano inayotumika ni Kiswahili na huzungumzwa kote Afrika Mashariki. Kiingereza kinatumika kama lugha ya kimataifa na kwenye biashara.

Uinjilishaji

Kihistoria uinjilishaji kwenye Jimbo Kuu Katoliki Arusha ulianza mwaka 1926 Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu kutoka Kanda (Vicariate) ya Kilimanjaro walipofungua vituo vya kitume sehemu inayoitwa “Mesopotamia” ilipo sasa Parokia ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu (Parokia Kuu ya Jimbo). Mwaka wa 1939 walifungua kituo kingine pale Usa River kikifuatiwa na Monduli mwaka 1953. Mwaka 1961 kituo kingine kilifunguliwa pale Emboreet, Simanjiro, kikifuatiwa na Kijungu mwaka 1962. Vituo hivi vya utume viliunda Jimbo la Arusha mwaka 1963 likitambuliwa rasmi kikanisa chini ya uongozi wa Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu kutoka Amerika. Marehemu Mhashamu Askofu Dennis Vincent Durning ambaye alianzisha Kituo cha Utume cha Loliondo alichaguliwa kuwa Askofu wa kwanza mwaka 1963.

Uongozi wa Jimbo tangu kuzinduliwa kwake

Tangu kuanzishwa kwake Jimbo Kuu Katoliki Arusha limeongozwa na maaskofu wanne kama ifuatavyo:-

  1. 1 Machi 19636 Machi 1989:      

Mhashamu Askofu Dennis Vincent Durning, C.S.Sp.

  1. 6 Machi 1989 – 20 Julai 1998:      

Mhashamu Askofu Fortunatus M. Lukanima

  1. 28 Novemba 1998 –  27 Disemba 2017:

Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Louis Lebulu

  1. 27 Disemba 2017 hadi leo :

Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani

Utendaji wa Jimbo Kuu

Mafanikio

Jimbo Kuu Katoliki Arusha linajivunia kuwa na waumini waliobatizwa wapatao 537,613, mapadri na watawa 391 pamoja na Makatekista 370.

Tangu kuanzishwa kwake, Jimbo Kuu Katoliki Arusha limeshuhudia mafanikio kadhaa yakiwemo kuongezeka kwa idadi ya Wakatoliki, na hadi sasa wamefikia 537,613 ambayo ni asilimia 31.7% ya wakaazi wote wa Mkoa wa Arusha ambao una wakaazi 1,694,310 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012. Mafanikio mengine yameonyeshwa kwenye jedwali la kwanza hapo chini.

Mwelekeo wa mafanikio ya Jimbo Kuu la Arusha

 Mwaka201420152016201720182019202020212022
Waumini wabatizwa  535,996  536,993  537,160  537,363  537,613    
Mapadri wazawa  49  49  49  51  54      78  82
Watawa wazawa  81  93  82  74  86    
Parokia444852545555555555
Dekania558888888

Kwa wakati huu Jimbo Kuu linatoa huduma mbali za kijamii zikiwemo Elimu, Afya, Maji safi na salama pamoja na huduma mbali kwa wahitaji. Huduma zote hizi huchangia kwa sehemu kubwa katika ukuaji wa jamii ya Kitanzania kwenye maeneo ya kiroho, kijamii na kiuchumi. 

Jimbo Kuu limeanzisha na kudumisha mahusiano mazuri ya kikazi kati ya jamii na wadau wengine. Kuwepo kwake, huduma na mahitaji yake vinatambuliwa na serikali, wanufaika na washirika wa maendeleo na wengine wote walio na mapenzi mema katika kuhudumia wale wote walio kwenye hali ya haja muhimu.