MKUU WA MKOA WA ARUSHA, PAULO CHRISTIAN MAKONDA, ATATUA MGOGORO KATI YA SERIKALI NA KANISA KATOLIKI ARUSHA ULIODUMU KWA TAKRIBAN MIAKA 30
Katika hatua ya kihistoria, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, akiwa na viongozi wa wilaya, wametekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukabidhi hati ya kiwanja cha Kanisa Katoliki Arusha ambacho kwa zaidi ya miaka 30 viongozi na waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakikihangaikia ili kukirejesha mikononi mwao.
Kiwanja hicho, chenye ukubwa wa takriban mita za mraba 7,503, kilikuwa chini ya umiliki wa Kanisa Katoliki Arusha na kilitumiwa na Jeshi la Polisi. Eneo hilo lilikuwa awali sehemu ya Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto wa Yesu, Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Mgogoro huu wa muda mrefu uliamuliwa baada ya kufikishwa kwa Rais Samia kupitia kwa RC Makonda na Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa. Rais Samia alitoa maagizo ya kurejeshwa kwa eneo hilo pamoja na kiasi cha shilingi milioni 500 ambazo zilikuwa mali ya Kanisa.
Akikabidhi eneo hilo tarehe 17 Oktoba 2024, kwa niaba ya Rais Samia, RC Makonda alisisitiza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya mgogoro wa muda mrefu kufikishwa kwa Rais na Waziri wa TAMISEMI. Serikali ilichukua hatua ya kurejesha eneo hilo baada ya kutambua haki ya Kanisa Katoliki juu ya umiliki wake.
Kwa upande wake, Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Mha. Isaac Amani, alimshukuru Raisi Samia Suluhu Hassan pamoja na uongozi wa serikali, akiwemo RC Paul Makonda, kwa juhudi zao za kutatua changamoto za wananchi. Pia alikemea tabia ya ubinafsi, ubabe na ulafi miongoni mwa watumishi wa umma wasiokuwa waaminifu.
Aliwaasa wananchi kutafuta amani na kudumisha umoja ndani ya jamii, huku akikemea unyanyasaji dhidi ya watu wa hali ya chini. “Sisi sote tuishi kwa upendo kwani ni watoto wa Baba mmoja, Mungu wetu wa mbinguni,” alisema Mhashamu Baba Askofu.