MISA TAKATIFU YA SIKUKUU YA MT. THOMAS WA AKWINO YAFANYIKA KATIKA SEMINARI YA MTAKATIFU THOMAS WA AKWINO OLDONYO SAMBU
Arusha, 28 Januari 2025 – Kanisa Katoliki kote ulimwenguni leo linaadhimisha sikukuu ya Mtakatifu Thomas wa Akwino, Padre na Mwalimu wa Kanisa. Katika Jimbo Kuu Katoliki Arusha, adhimisho hili limefanyika kwa namna ya pekee katika Seminari ya Mtakatifu Thomas wa Akwino iliyopo Oldonyosambu ambapo yeye ndiye somo na msimamizi wa seminari hiyo.
Misa Takatifu ya sikukuu hii imeongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Isaac Amani, akishirikiana na mapadre wa jimbo hilo. Katika adhimisho hili, pia kulikuwa na sherehe ya kuwaaga wanafunzi wa kidato cha nne pamoja na kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tano, huku Askofu Mkuu Isaac Amani akiwahimiza wafuate mfano wa Mtakatifu Thomas wa Akwino kwa kumtumikia Mungu kwa utume wa elimu na imani.
“Wanaseminari wote waishi maisha kama ya Mtakatifu Thomas wa Akwino, ambaye alijitoa katika utume wake kwa kumtumikia Mungu, hasa kupitia upadre na maandiko yake mbalimbali. Mtakatifu Thomas wa Akwino alikuwa mwandishi hodari wa vitabu vya theolojia na mtunzi wa nyimbo za Kanisa. Hivyo basi, ninyi pia mhimizwe kuishi Ukristo wenu kwa upendo na kusaidiana, kama tunavyoagizwa katika Injili ya Yohane 13:34-35: ‘Amri mpya nawapa, mpendane kama nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Watu wote watatambua kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi’,” alisema Askofu Isaac Amani.
Katika mahubiri yake, Askofu Amani aliwasihi waseminari wote kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo, akisema kuwa wafuasi wa Kristo siku zote huwa tayari kuwa karibu na Bwana ili waweze kulishwa kiroho, kama vile wanafunzi wa Yesu walivyokuwa karibu naye.
Mtakatifu Thomas wa Akwino: Mwalimu wa Kanisa
Mtakatifu Thomas wa Akwino alizaliwa mwaka 1225 nchini Italia. Alifariki dunia tarehe 7 Machi 1274 akiwa njiani kuelekea Mtaguso wa Lioni. Alitangazwa kuwa mtakatifu na Papa Yohane XXII mnamo tarehe 18 Julai 1323. Kutokana na mchango wake mkubwa katika teolojia na falsafa ya Kikristo, alipewa heshima ya kuwa Mwalimu wa Kanisa tarehe 11 Aprili 1567 na Papa Pio V.
Katika maisha yake, alijitolea kwa masomo na maandiko, akiacha urithi mkubwa wa mafundisho ya imani. Kwa muktadha huu, Askofu Amani aliwataka waseminari na waumini wote kumchukua Mtakatifu Thomas wa Akwino kama mfano wa kumfuata katika safari ya imani na kujitoa kwa Mungu. “Hivyo basi, sote twaweza kuishi kwa uaminifu, upendo kwa Kristo na kwa jirani zetu ili kufikia utakatifu kama watakatifu wengine. Tukumbuke kuwa msingi wa maisha yetu ya Kikristo ni Ekaristi Takatifu,” alihitimisha Askofu Amani.
Sikukuu hii ya Mtakatifu Thomas wa Akwino ni fursa kwa waumini kutafakari juu ya maisha ya utakatifu na kujituma katika kumtumikia Mungu kwa vipaji walivyojaliwa, kama alivyofanya Mtakatifu huyu mashuhuri wa Kanisa Katoliki.