UZINDUZI WA NYUMBA YA MAPADRI PAROKIA YA MOYO MTAKATIFU WA YESU, SOMBETINI – JIMBO KUU KATOLIKI ARUSHA
Uzinduzi wa nyumba ya mapadri katika Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Sombetini, ulifanyika kwa heshima kubwa tarehe 18 Januari 2025. Sherehe hiyo ilihusisha adhimisho la Misa Takatifu ilioyoongozwa na Askofu Mkuu Isaac Amani, akiambatana na Askofu Mkuu Mstaafu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha,
Askofu Mkuu Isaac Amani alimshukuru Mungu kwa kukamilika kwa nyumba hiyo na kuiombea iwe baraka kwa utume wa Kanisa na mapadre wote watakaoitumia. Pia, alimpongeza Paroko wa parokia hiyo, Padri Prosper Tesha, kwa uongozi thabiti na usimamizi mzuri wa mradi huo, pamoja na waumini wote na wale wenye mapenzi mema waliotoa michango yao kutoka ndani na nje ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha.
Wito kwa Waumini
Katika homilia yake, Askofu Mkuu Amani aliwataka waumini wote kuheshimu Neno la Mungu, akisisitiza kuwa:
“Neno la Mungu lina nguvu na ukali kuliko kitu chochote. Msilidharau, bali lisomeni kila siku kwa maana ndilo nguzo ya maisha ya kila Mkristo.”
Aliwahimiza waumini kukumbuka huruma kuu ya Mungu inayopatikana kupitia Kristo Yesu, ambaye ni kipatanisho cha dhambi za ulimwengu. Alihusianisha mafundisho hayo na mwaka wa Yubilei Takatifu 2025 wenye kaulimbiu: “Mahujaji katika Matumaini: Neno la Mungu likae ndani yetu.” Akirejelea Mathayo 11:28, alisema:
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”
Tahadhari kwa Nyumba za Mapadri
Askofu Mkuu pia aliwakumbusha watawa na waumini umuhimu wa kuheshimu nyumba za mapadri, akisisitiza kuwa nyumba hizo zimewekwa wakfu kwa ajili ya mapadre kufanya kazi ya kiroho na mazungumzo na Kristo. Alionya dhidi ya kuruhusu kila mtu kuingia bila sababu za msingi.
Maadili na Utii wa Sheria za Mungu
Katika hitimisho lake, Askofu Mkuu aliwahimiza waumini kushika sheria za Mungu na Kanisa, akiwakumbusha kuwa:
“Miili yetu ni hekalu la Mungu. Acheni uzinzi, masengenyo, ubadhirifu wa mali na tamaa zisizofaa, kwa kuwa mambo haya hayampendezi Mungu na huleta mafarakano katika jamii zetu.”
Sherehe hiyo ilikuwa kielelezo cha mshikamano wa kiimani na mafanikio ya ushirikiano baina ya viongozi wa Kanisa na waumini katika kutimiza miradi ya kichungaji.
Mungu ibariki Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Sombetini