Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, ni wa awamu ya nne kuongoza na wa Pili tangu Jimbo la Arusha kupandishwa hadhi na kuwa Jimbo kuu katoliki Arusha . Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani alizaliwa Juni 10, 1951, Kijiji cha Mloe Parokia ya Mango Jimbo la Moshi. Alisoma Shule ya Msingi Mango, baadaye Seminari ndogo ya Mt. Yakobo Jimbo la Moshi, baadaye masomo ya Falsafa Seminari Kuu ya Ntungamo 1970 – 1972 na Teolojia katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Jimbo Kuu la Tabora. (1972-1975). Alipewa daraja ya Upadre Jimbo la Moshi, tarehe 29 Juni 1975 na tangu wakati huo amehudumu kama ifuatavyo: 1975-1976: Paroko Msaidizi huko Narumu; 1976-1979: Paroko Msaidizi huko Moshi Kathedrali; 1980-1986: Mwalimu na Makamu Gombera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yakobo, Moshi; 1986-1989: Mafunzo ya Elimu na Ushauri wa Kichungaji katika Chuo Kikuu cha Walsh, Ohio, U.S.A.; 1990-2003: Padre na Mlezi wa Shirika la Mabruda wa Mkombozi Jimbo la Moshi, 1999-2004: mjumbe wa maaskofu kwa ajili ya Watawa na tangu Julai 2003, Paroko Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Moshi. Tarehe 21 Novemba 2007, aliteuliwa na Papa Benedict XVI kuwa Askofu wa Moshi na kuwekwa wakfu tarehe 22 Februari 2008. Desemba 27, 2017 Papa Francisko alimteua Mhashamu Isaac Amani Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha na kusimikwa tarehe 8 Aprili 2018.