MAISHA YA AWALI NA WITO WA UPADRI
Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani alizaliwa tarehe 10 Juni 1951 katika Kijiji cha Mloe, Parokia ya Mango, Jimbo la Moshi. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mango, kisha akaendelea na masomo ya seminari ndogo ya Mtakatifu Yakobo Jimbo la Moshi. Baadaye, alisomea falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo (1970 – 1972) na teolojia katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Jimbo Kuu la Tabora (1972 – 1975). Alipadrishwa tarehe 29 Juni 1975 katika Jimbo la Moshi.
SAFARI YA KICHUNGAJI NA UONGOZI
Baada ya kupadrishwa, alihudumu kama Paroko Msaidizi katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Narumu (1975 – 1976) na Moshi Kathedrali (1976 –1979). Kati ya mwaka 1980 hadi 1986, alihudumu kama Mwalimu na Makamu Gombera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yakobo, Moshi. Aliendelea na masomo ya elimu na ushauri wa kichungaji katika Chuo Kikuu cha Walsh, Ohio, Marekani (1986 – 1989). Baada ya kurejea, alihudumu kama Padre na Mlezi wa Shirika la Mabruda wa Mkombozi Jimbo la Moshi (1990 – 2003) na pia alikuwa Paroko wa Kanisa Kuu la Kristo Mfalme, Moshi kuanzia Julai 2003.
UASKOFU NA UASKOFU MKUU
Tarehe 21 Novemba 2007, aliteuliwa na Papa Benedict XVI kuwa Askofu wa Moshi na kuwekwa wakfu tarehe 22 Februari 2008. Baadaye, tarehe 27 Desemba 2017, Papa Francisko alimteua kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha na alisimikwa rasmi tarehe 8 Aprili 2018.
MAADHIMISHO YA JUBILEI YA MIAKA 50 YA UPADRI
Maadhimisho haya ya Jubilei ya Miaka 50 ya Upadri wa Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani ni fursa ya kutafakari na kusherehekea maisha ya huduma ya kiroho na uongozi uliotukuka. Ni wakati wa waumini na jamii kwa ujumla kumshukuru Mungu kwa zawadi ya kiongozi huyu na kuendelea kumuombea afya njema na nguvu katika kuendeleza utume wake.
Kwa maelezo zaidi kuhusu historia na huduma ya Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, unaweza kutembelea tovuti rasmi ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha