Hakufanya ibada hizo za kichungaji peke yake bali aliwashirikisha makatekista wengi kutoka Moshi ili kumsaidia katika kueneza Neno la Mungu katika maeneo mbalimbali ya Loliondo. Katika kazi zote, alipendelea kushirikiana na walei ili kuifanya idumu. Katika maisha yake yote alitaka walei wahusishwe katika kuujenga Ufalme wa Mungu. Alihudumu katika shughuli za kichungaji/misheni Loliondo hadi alipochaguliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Arusha. Aliwekwa wakfu na Askofu Mkuu wa Philadelphia tarehe 28-05-1963 na baadaye kusimikwa katika Jimbo la Arusha na Askofu Del Mestri, Mwakilishi wa Papa tarehe
08-09-1963. Katikati ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vaticano mwaka 1963, ni mwaka ambao Jimbo Katoliki la Arusha lilipoanzishwa.
Safari hii ilikuwa na athari kubwa kwa Jimbo kwani Askofu alilazimika kuondoka mara moja kwenda kuungana na maaskofu wenzake katika baraza hilo. Pili, mawazo na matendo ya Sinodi yalilenga katika maendeleo ya Jimbo jipya, hasa liturujia, teolojia, kazi ya kitume na uhusiano na madhehebu mengine. Askofu alitambua wazi kwamba huduma ya Kanisa ni kwa ajili ya kuwakuza wanadamu kwa ujumla, hivyo Askofu alisisitiza sana utume wa walei wa kuanzisha Parokia. Kwa mtazamo huo makatekista, walihitaji elimu bora na huduma ya afya. Askofu Dennis Durning katika maneno yake anasema “Tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatikano na kuanza kwa Jimbo letu Wakristo wanapaswa kuelimishwa juu ya wajibu wao na mwamko wa kazi yao ya kitume. Tunataka wengi wawe mitume katika familia, katika jumuiya, na katika mazingira yao ya kila siku. Isipokuwa tutakuwa na aina hii ya juhudi zetu zote zitakuwa bure.
Alipokuwa Askofu wa Arusha mwaka 1963 kulikuwa na parokia nne (4) tu. Parokia hizi ni Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Parokia ya Usa River, Parokia za Monduli na Loliondo. Kulikuwa na mapadre wawili (2) wa jimbo na watawa na wamisionari kumi na wawili (12), washiriki wa Shirika la Roho Mtakatifu, na watawa wa kike wanne (4) na washirikia wa Damu Takatifu.
Tunapoadhimisha kifo chake kila mwaka, tunatoa shukrani zetu kwa Mungu kwa maisha na kujitolea kwake kama Padre na Askofu wa Jimbo letu la Arusha. Licha ya kukuza utume wa makatekista jimboni, aidha alianzisha Seminari Ndogo (Mt. Thoma wa Akwino) huko Oldonyo Sambu ili kulea vijana wa kiume kuwa mapadre wa jimbo ambao wangetumikia Kanisa mahalia. Aliwakaribisha watawa wanaume na wanawake ili kuendeleza utume wa kichungaji, ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za malezi na kuwashirikisha waamini katika miito ya kipadre na kitawa. Aliwakaribisha walei kutoka nje ya nchi (Marekani na Ulaya) kusaidia Jimbo katika nyanja mbalimbali. Mnamo Desemba 2017 Jimbo ilimkumbuka kwa kumbukizi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Seminari yetu Ndogo ya Oldonyo Sambu. Alihudumu katika Jimbo la Arusha kwa miaka 26 na wakati huo parokia ziliongezeka hadi 24, na mapadre wa Jimbo wapatao 22. Mwaka 1989 Askofu Dennis Vincent Durning alistaafu na baada ya miaka 13 alifariki tarehe 23.02.2002 ili kuungana na Mungu.
Askofu Dennis Durning alijulikana kuwa mtu ambaye alijikana mwenyewe kwa maisha yake ya upendo, unyenyekevu na furaha. Huko Loliondo na Sonjo mara nyingi alikuwa akisafiri kwa Punda kwani siku hizo hakukuwa na barabara. Alijishusha na kujifunza utamaduni wa watu wa hapa Arusha. Askofu Durning atakumbukwa kwa upendo wake kwa walei na kushiriki katika kuujenga mwili wa Kristo.
Kila tunapoadhimisha kumbukizi ya kifo chake, inafaa sana kutafakari maisha yake na kumkumbuka. Akiwa mwanzilishi wa Jimbo letu, alipanda mbegu nzuri na sasa tunaendelea kuona matunda yake. Tuendelee kuiga mfano wake na kumwomba atuombee kwa Mungu ili tuendelee kumshuhudia Mungu.
Nembo ya Kwanza ya Utume wa Jimbo la Arusha

“NITAKULISHA KATIKA MALISHO MEMA”
Nembo ya Kimisionari ya Kiaskofu katika Papa wa Askofu Dennis Vincent Durning ni “IN PASCUIS UBERRIMIS PASCAM EAS. Kwa hakika maisha na utume wake wote ulionyesha Roho hii ya Utume. Tufuate mfano huu katika maisha yetu kama Mapadre, watawa na walei. Tuendelee kuwalisha kondoo wazuri tuliokabidhiwa.