Askofu Dennis Vincent Durning alizaliwa Philadelphia, Marekani tarehe 18-05-1923. Alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto watano katika familia yake. Aliingia katika Usharika wa Roho Mtakatifu tarehe 16-07-1937 na baada ya miaka kadhaa ya masomo ya seminari, akapewa daraja la Upadre tarehe 03-06-1949. Mwaka 1950 alianza misheni katika Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania. Alifanya utume hasa maeneo ya Mashati na Rombo. Baada ya utume wake wa kichungaji kwa miaka sita alihamishwa kwenda kutumikia Kanisa la Loliondo ambako alihudumia Jumuiya ya Wamasai na Wasonjo. Pia alijikita katika kukuza ubinadamu kiujumla, hivyo akajenga Hospitali za Wasso na Endulen, Zahanati za Soit Sambu na Sonjo, pamoja na shule zinazosimamia Ngorongoro, Kakesio na Nainokanoka.