Become A Donor

Become A Donor
Lorem Ipsum is simply dummy text of the printing and typesetting industry.

Contact Info

684 West College St. Sun City, United States America, 064781.

(+55) 654 - 545 - 1235

info@zegen.com

KANISA JIPYA LA FAMILIA TAKATIFU NJIRO LAWA FAHARI YA JIMBO KUU KATOLIKI ARUSHA

KANISA JIPYA LA FAMILIA TAKATIFU NJIRO LAWA FAHARI YA JIMBO KUU KATOLIKI ARUSHA

ALAMA YA UJENZI WA IMANI, UPENDO NA UMOJA WA KIKRISTO

Na Apolinary P. Shiyo
Idara ya Mawasiliano, Jimbo Kuu Katoliki Arusha

Kauli mbiu ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha, “Kujitambua, Kuwajibika na Kushirikiana katika Kristo kwa Matendo”, imeendelea kuwa dira ya kuongoza safari ya kiroho na kimwili ya waamini wake. Kupitia mwanga wa kauli mbiu hii, Jimbo limezidi kuimarisha imani, upendo na mshikamano, matokeo ambayo yanaonekana wazi katika tukio la kihistoria la kutabarukiwa kwa Kanisa Jipya la Familia Takatifu Njiro, alama hai ya umoja na uthabiti wa waamini wa Arusha.

Siku ya Shukrani na Furaha

Jumamosi, tarehe 11 Oktoba 2025, itabaki kuwa kumbukumbu ya furaha na shukrani katika historia ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Siku hiyo, Askofu Mkuu Isaac Amani aliongoza Ibada Takatifu ya Kutabaruku Kanisa Jipya la Familia Takatifu Njiro, lililojengwa upya baada ya kubomolewa kwa lile dogo la awali. Tukio hilo lilihudhuriwa na mapadre wa Jimbo, watawa wa mashirika mbalimbali, waamini kutoka ndani na nje ya Jimbo, pamoja na wageni waalikwa.

Nyuso za furaha, nyimbo za shukrani na machozi ya faraja vilitawala anga la Njiro, kila mmoja akimtukuza Mungu kwa matendo makuu aliyowatendea.

Paroko wa sasa, Padre Benedikti Ole Kashe, amekuwa nguzo kuu ya mafanikio haya. Kupitia uongozi wake wa kiuchungaji, bidii na maombi ya waamini, ujenzi wa Kanisa hili umekuwa si tu kazi ya mikono, bali ni matokeo ya imani hai na moyo wa upendo wa kindugu.

Historia Fupi ya Parokia ya Njiro

Parokia ya Familia Takatifu Njiro ilianzishwa mwaka 1990 na Padre Richard De Clair (CSSp), ambaye sasa ni marehemu. Tangu wakati huo, Parokia imeongozwa na wachungaji mbalimbali walioweka alama katika ukuaji wa kiimani na maendeleo ya miundombinu  akiwemo Padre Fidelis Tamamu (marehemu), Padre Joseph Babu CSSp (marehemu) na Padre Austaki Tarimo kabla ya uongozi wa sasa wa Padre Benedikti Ole Kashe.

Ujenzi wa Kanisa Jipya: Alama ya Imani na Umoja

Mradi huu wa ujenzi umechukua kipindi cha miaka mitatu na nusu pekeem ushuhuda wa bidii na ushirikiano wa waamini wa Parokia ya Njiro. Muundo wa Kanisa unaakisi ubunifu wa kisasa uliochanganywa na urithi wa Kikatoliki, ukiwa mfano wa sanaa, imani na umoja.

Kanisa hili jipya ni miongoni mwa makubwa zaidi katika Jimbo, likiwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya waamini 1,500 kwa wakati mmoja. Ndani yake kuna ofisi za kichungaji na kapela dogo (chapel) lililoko sakafu ya chini kwa ajili ya sala na tafakari binafsi.

Kupitia kazi hii, waamini wa Njiro wameonyesha kwa vitendo maana ya kauli mbiu ya Jimbo kujua nafasi yao ndani ya mwili wa Kristo, kuwajibika kwa matendo ya upendo, na kushirikiana kwa moyo wa imani.

Wosia wa Baba Askofu Mkuu Isaac Amani

Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu Isaac Amani aliwataka waamini wa Parokia ya Familia Takatifu Njiro kuishi mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu familia ya imani, utiifu na upendo.

Alisisitiza kuwa jina la Parokia linabeba wajibu wa kuwa kioo cha maadili na mshikamano katika jamii. Kila familia, alisema, inapaswa kuwa “kitalu cha miito mitakatifu” na “shule ya maadili” kwa Kanisa na Taifa kwa ujumla.

“Ujenzi wa Kanisa hauishii kwenye mawe na saruji, bali unaendelea kila siku katika mioyo yenu,” alisema Askofu Mkuu Amani. “Kujenga maisha yenu kwa Kristo ndiko kujenga Kanisa hai.”

Shukrani na Mwito wa Kuendeleza Ujenzi wa Imani

Katika hotuba yake ya shukrani, Askofu Mkuu Amani aliwapongeza waamini wote wa Parokia ya Njiro kwa moyo wa kujitolea na sadaka zao za hali na mali. Alimpongeza pia Paroko, Padre Benedikti Ole Kashe, kwa uongozi wake thabiti, hekima na moyo wa uchungaji uliowezesha mafanikio haya.

Aliwaalika waendelee kudumisha umoja, sala na upendo, ili Kanisa hilo liwe kweli nyumba ya sala na chemchemi ya imani hai.

Ushuhuda wa Imani Hai

Tukio la kutabaruku Kanisa Jipya la Familia Takatifu Njiro limeacha alama ya kudumu katika historia ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Ni ushuhuda wa nguvu ya imani, moyo wa ushirikiano na kujitolea kwa dhati chini ya dira ya “Kujitambua, Kuwajibika na Kushirikiana katika Kristo kwa Matendo.”

Kupitia mafundisho na wosia wa Askofu Mkuu Amani, waamini wa Parokia hii wameitwa kuendelea kuwa mashahidi wa imani hai, wakiishi mfano wa Familia Takatifu  Yesu, Maria na Yosefu  kama kielelezo cha upendo, utiifu na umoja katika Kristo.

 

🕊️ Kanisa Jipya la Familia Takatifu Njiro lililotabarukiwa na Askofu Mkuu Isaac Amani, ni alama ya Imani Thabiti, Upendo wa Kikristo na Umoja unaokua  ishara ya mafanikio ya Kauli Mbiu ya Jimbo Kuu Katoliki Arusha: “Kujitambua, Kuwajibika na Kushirikiana katika Kristo kwa Matendo.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked*