KONGAMANO LA 5 LA EKARISTI TAKATIFU TANZANIA LAHITIMISHWA KWA MISA TAKATIFU
Adhimisho hilo la kilele liliendeshwa na Askofu Wolfgang Pisa wa Jimbo la Lindi, ambaye pia ni Raisi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Askofu Pisa aliwaasa waamini wote nchini kuishi kwa upendo na kutokubaguana kwa misingi ya rangi, udini au ukabila, akisisitiza kuwa sisi sote ni ndugu mbele ya Mungu. Alisisitiza kwamba Sakramenti ya Ekaristi ni chanzo cha uzima, hivyo waamini wanapaswa kuijongea wakiwa wasafi kiroho na wakiwa katika hali ya kiungu.
Askofu Wolfgang aliendelea kwa kusema, “Ekaristi inapaswa kuwa kipatanisho cha upendo na mshikamano katika jamii, kuondoa tofauti za kidini, kikabila, na uvunjifu wa amani. Tufanye kazi kwa pamoja ili kudumisha umoja wetu kama ndugu.”
Naye Balozi wa Papa Francisko nchini Tanzania, Askofu Angelo Accattino, aliwasilisha salamu za Papa Francisko kwa waumini waliohudhuria kongamano hilo, akisema kuwa Baba Mtakatifu ameungana nao kwa sala katika kumalizia Kongamano hilo. Alipongeza maandalizi mazuri ya Kongamano hilo na kumshukuru Mungu kwa neema za Ekaristi.
Viongozi wa serikali walioshiriki katika tukio hilo, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati, Mh. Dotto Biteko, waliwashukuru maaskofu kwa maandalizi yao bora na kuhimiza waumini waendelee kuombea amani ya taifa. Walimwomba Yesu Kristo awe mlinzi wa amani na umoja nchini Tanzania.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwaichi, aliwapongeza waumini, maaskofu na watawa kwa kujitokeza kwa wingi katika Kongamano hilo. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza amani, ambayo ni tunu kubwa kutoka kwa Mungu. Aidha, aliwapongeza waumini wa Arusha kwa kujiandaa kwa Kongamano la 6 la Ekaristi Takatifu, kama lilivyotangazwa na Askofu Wolfgang Pisa.
Misa ya ufunguzi wa kongamano hili iliadhimishwa na Askofu Mkuu Jude-Thadeus Ruwa’ichi tarehe 12 Septemba 2024, ikishuhudia umati mkubwa wa waumini. Kongamano hili pia liliambatana na hitimisho la Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo nchini Tanzania.