Arusha, Tanzania – Julai 10, 2025
Katika tukio adhimu na lenye mvuto wa kiimani, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Arusha limezidi kung’aa kwa neema ya Daraja Takatifu la Upadre, ambapo Mashemasi 16 kutoka mashirika mbalimbali pamoja na wa Jimbo walipewa daraja hilo takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Kanisa Kuu la Jimboni Arusha. Akiongoza Adhimisho la Ekaristi Takatifu, Mhashamu Isaac Amani, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Arusha, aliwatolea wito maalum Mapadre wote kutimiza kwa uaminifu na bidii kazi ya Kikuhani wakiwa ni wawakilishi wa Kristo, Mchungaji Mwema, katika dunia hii yenye changamoto lukuki za Kiroho na Kimaadili.
“Yesu Kristo ndiye Mchungaji Mwema. Nanyi Mapadre mmetiwa wakfu ili kuitimiza kazi hiyo hapa duniani kwa niaba yake kwa kuwafundisha watu ukweli, kuwaongoza kwa Kristo, kuwabatiza wasiobatizwa, kuwasaidia watu waijue Injili, na kuwaandaa kwa Ndoa Takatifu. Ndoa ndiyo kitalu cha miito yote pasingekuwepo ndoa, ninyi pia msingekuwepo” alisisitiza Mhashamu Amani huku akihimiza utakatifu wa maisha ya Kipadre.
Katika tukio hilo, lililohudhuriwa na maaskofu wanne, miongoni mwao ni Askofu Msaidizi Prosper Lyimo wa Jimbo Kuu Arusha, Askofu Henri Mchamungu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Askofu Mstaafu Josephat Louis Lebulu.
Askofu Mkuu Isaac Amani alikazia kwamba Mapadre ni taa ya ulimwengu wa sasa, wakipaswa kutembea katika mwanga wa Kristo na kutoyumbishwa na mambo ya muda mfupi bali waishi kwa ajili ya maisha ya milele. “Sisi si wa dunia hii. Uhuru wetu usitufikishe kwenye maangamizi bali utupeleke kwenye Utakatifu. Tumuombe Mungu atuwezeshe kudumu katika mwanga wake. Tumsumbue shetani kwa kusali, maana akivuruga Mapadre, amevuruga kondoo wote wa Kristo” alionya kwa msisitizo mkubwa. Aidha, Mhashamu Isaac Amani aliwakumbusha wazazi kuwa sehemu muhimu ya malezi ya miito ya kitawa na kipadre, akisema malezi mema yanahitaji uvumilivu, upole na sala ya kudumu. “Wazazi mna nafasi ya pekee. Mtoto anayetamani kuitikia wito wa Mungu anatakiwa ajue udhaifu wake kama binadamu na aendelee kusali ili neema ya Mungu imwezeshe kuufikia wito wake” alieleza kwa upole wa kichungaji. Katika ujumbe wake kwa taifa, Askofu Mkuu Amani hakusita kuzungumzia changamoto ya utandawazi na athari zake kwa jamii, hasa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. “Watu wengi wanaugua ‘homa ya utandawazi’. Wamekosa muda wa kufanya kazi na kupoteza utulivu wa akili. Tuutazame utandawazi kama chombo cha maendeleo na si chanzo cha mporomoko wa maadili” alionya kwa hekima.
Mwishoni mwa mahubiri yake, Askofu Mkuu aliwahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuombea uchaguzi mkuu ujao wa mwezi Oktoba 2025, ukapite kwa haki, amani na uchaguzi wa viongozi waadilifu. “Tumuombe Mungu atupe viongozi wenye maadili, wazalendo wa kweli watakaotetea maslahi ya wananchi na si ya kwao binafsi. Taifa linahitaji viongozi wa moyo safi,” alihitimisha kwa uzito wa kinabii. Katika hali ya kipekee, adhimisho hilo lilijawa na furaha, shangwe, nyimbo Takatifu na moyo wa mshikamano wa kiroho, ishara ya muendelezo wa Kanisa la Kristo kukua na kuzaa matunda kupitia huduma takatifu ya Upadre.
Na kwa utukufu wa Mungu, Kanisa linaendelea kupokea watumishi wapya, wakfu kwa huduma na sadaka, kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.